Monday, March 11, 2013

Aibu,vyoo vya shule karne ya 21

Choo cha shule 
Kwa ufupi
Tafiti zabainisha shule nyingi nchini zina vyoo duni sana  ukilinganisha na mataifa mengine Afrika Mashariki. Wasomi wasema vyoo visivyofaa huchangia maendeleo mabaya kwa watoto wa kike hasa waliovunja ungo, kwa vile hushindwa kujisitiri vizuri wanapokuwa hedhi, hivyo kusababisha baadhi yao kutokwenda shule.
Wanafunzi wa kike hulazimika kuomba huduma za kujisaidia kwenye vyoo vya karibu na shule, huko baadhi yao wanabakwa au kufanyiwa ukatili mwingine wowote


Huduma za vyoo katika shule mbalimbali nchini inaonekana mbaya kiasi cha kutishia uhai wa wanafunzi na walimu wanaovitumia.
Wataalamu wa masuala ya elimu na saikolojia, wanaibainisha pia kuwa vyoo vinapokuwa duni, vinachangia kudumaza maendeleo sekta ya elimu kwa sababu wanafunzi wenye kuhara, kwa mfano au wa kike hulazimika kutokwenda shule hasa wanapokuwa hedhi kwa vile wanashindwa kujisitiri.
Shule ina wanafunzi 400 haina vyoo
Shule ya Msingi Lugalo iliyopo Kata ya Mazombe, wilayani Kilolo mkoani Iringa yenye zaidi ya wanafunzi 400 ni kati ya shule ambazo kwa miezi mitatu hivi mfululizo  imekuwa ikielezwa kutokuwa na vyoo thabiti, achilia mbali uhaba mkubwa wa madawati, kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joseph Kinyanya.
Shule ina matundu 16 ya vyoo vilivyojengwa kwa miti, ambayo imeoza, mwalimu huyo mkuu ana hofu huenda ikafungwa kwa kuonekana kama eneo lisilo salama kwa watoto, kwani wanaweza kupoteza maisha kwa kutumbukia chooni. Kati ya shule 96 za msingi za wilaya hiyo, Lugalo mara kadhaa imekuwa ikishika nafasi ya tano, hata hivyo Mwalimu Kinyanya, ana hofu huenda maendeleo haya yakawa mabaya ikiwa mazingira hayataboreshwa haraka.
Watafiti wabainisha
Ripoti iliyotolewa mapema mwezi huu na Shirika la Water Aid, lenye ofisi nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, inaonyesha kuwa hali ya vyoo katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, inasikitisha, huku watoto wa kike wakielezwa kuathirika zaidi kutokana na maumbile yao kuhitaji zaidi usafi hasa wanapokuwa hedhi.
Mkataba wa Dakar wa elimu kwa wote, unataka ifikapo mwaka 2015 watoto wote wawe wana uwezo wa kupata elimu ya msingi iliyo bora ikiwamo kuwa na uhakika wa huduma za vyoo na mazingira ya shule kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa hali inavyoonekana ni ndoto au huenda ikachukua kazi ngumu mno kwa Tanzania kutimiza hilo, kutokana na kubainika kuwa na shule nyingi kutokuwa na vyoo thabiti, zikiwamo za mijini, achilia mbali za vijijini.
Hali mbaya ya vyoo shuleni
Ripoti hiyo inasema,  Shule ya Msingi Mpalanga iliyopo Chamwino mkoani Dodoma ina wanafunzi 1,022 huku ikiwa na matundu 10 tu ya vyoo, hivyo kusababisha wanafunzi kwenda chooni kwa foleni.
Choo cha matawi ya majani Shule ya Zejele
Hali kadhalika shule ya Zejele iliyopo Chamwino, mkoani Dodoma nayo vyoo vyake licha ya kujengwa kwa miti, imeezekwa kwa majani na udongo, huku milango ikiwa wazi, na baadhi ya vyoo vikiwa vinatumia milango ya matambala yaliyochakaa.
Jambo hili limekuwa likisababisha baadhi ya wanafunzi kujisaidia porini ambako angalau mtu anaweza asionekane anapojisaidia kuliko chooni.
Ili kuangalia kama vyoo vinasaidia kuimarisha ari ya watoto kusoma au la, WaterAid ilijenga vyoo vyenye matundu 20 hivi karibuni katika shule hiyo na katika utafiti walibaini kuwa kuwapo kwa vyoo vizuri vinachangia ongezeko la mahudhurio ya watoto shuleni.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Salvina Maswaga (12) anasema “Vyoo tulivyokuwanavyo mwanzo vilikuwa vibaya sana, kulikuwa hakuna milango, vilikuwa vidogo na vichafu, hivi vya sasa vinakufanya hata utamani kuja shuleni.”

No comments:

Post a Comment