Bradford City imewashangaza
wengi kwa kuilaza timu inayoshiriki katika ligi kuu ya Premier kwa
magoli 3-1, katika mechi ya raundi ya kwanza ya kuwania kombe la ligi.
Bradford iliilaza Aston Villa magoli hayo katika
uwanja wao wa nyumbani na hivyo kuimarisha matumaini yao ya kufuzu kwa
fainali ya kombe hilo kwa mara ya kwanza.
Timu
hiyo inayoshiriki ligi daraja ya pili, inashikilia nafasi sitini nyuma
ya Aston Villa katika orodha ya timu bora nchini Uingereza.
Aston Villa sasa itahitaji kuilaza Bradford City
kwa zaidi ya magoli mawili kwa bila katika mechi ya raundi ya pili ili
kufuzu kwa fainali hizo.
Kufikia wakati wa mapunziko, Bradford ilikuwa ikiongoza kwa bao moja kwa bila lililofungwa na Nahki Wells.
Kipa wa Bradford Matt Duke, alizuia makombora
makali kutoka kwa washambulizi wa Aston Villa waliokuwa wakiongozwa na
Christian Christian Benteke.
Baada ya kipindi cha pili kuanza, wenyeji
waliendeleza mashambulio yao na juhudi zao zilizaa matunda pale Rory
McArdle alipoifungia Bradford bao lake la pili dakika kumi na tatu kabla
ya mechi hiyo kumalizika.
Wachezaji wa Villa hawakufa moyo na waliendeleza
mashambulio yao na kupata bao lao la kwanza kupitia kwa mchezaji
Andreas Weimann.
Matumaini ya Villa ya kukomba bao la pili,
yalizimwa kabisa dakika chache baadaye na Carl McHugh ambaye aliifungia
Bradford bao lake la tatu kwa kichwa, baada ya kupokea pasi nzuri kutoka
kwa Gary Jones.
Ni dakika 90 pekee zimetenganisha Bradford na
fainali ya kombe hilo la ligi mwaka huu, lakini baada ya kuiondoa
Arsenal kwenye kinyanganyiro hicho, mashabiki wengi wanahisi kuwa huenda
timu hii inayoshiriki ligi ya chini, ikawashangaza wengi na kuibuka na
ushindi.
Ikiwa itafuzi kwa fainali hizo, Bradford itakuwa
imeandikisha historia ya kuwa timu ya kwanza tangu mwaka wa 1962, kwa
timu inayoshiriki ligi daraja la pili kufika fainali.
Mwaka huo timu ya Rochdale ilifuzu kwa fainali kinyume na matarajio ya wengi.
No comments:
Post a Comment