Wednesday, January 9, 2013

kimataifa/M23 wataka makubaliano na DRC



Msemaji wa kundi la waasi wa M23 Francois Rucogoza.
Waasi wa kundi la M23 katika Jamuhiri ya Kidemokrasia ya Congo, wametangaza kusitisha vita kabla ya awamu ya pili ya mazungumzo ya amani na serikali.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kampala, Uganda, waasi hao walisema kuwa wanatumai serikali nayo itafanya vivyo hivyo.
Jaribio la mwezi jana la kutafuta mwafaka, wa kumaliza vita vya miezi tisa mashariki mwa DRC liligonga mwamba.
Hadi watu laki nane, wameachwa bila makao tangu waasi walipoanza mapigano dhidi ya serikali mwezi Mei.
"sisi daima tumekuwa tukitaka amani. Leo, tunatangaza kuwa tumesitisha vita'' alisema msemaji wa kundi hilo, Francois Rucogoza.
"hata kama serikali itakataa kutia saini makubaliano ya amani, tutaendelea na mazungumzo'' aliongeza kusema bwana Rucogoza.

'Usaidizi wa Rwanda'

Waasi wa M23, wameituhumu serikali ya rais Joseph Kabila kwa kukosa kutii mkataba wa awali wa amani, kuweza kuwajumuisha waasi hao katika jeshi la serikali.
Waasi wa M23 wamekuwa wakipigana na wanajeshi wa DRC tangu mwezi Mei mwaka jana
Waasi wenyewe hata hivyo, walipiga hatua katika harakati zao mwaka jana. Waliuteka mji mkubwa wa Goma mwezi Novemba, lakini wakaondoka baada ya shinikizo kali za jumuiya ya kimataifa.
Aidha msemaji wa serikali Lambert Mende alisema kuwa serikali haina 'imani sana na mwafaka wa waasi hao.
"hatudhani kama tunaiona hatua ya waasi hawa kama yenye nia njema kutoka kwa watu ambao hawana nia ya kutenda kama wanavyosema. Tunatafakari mwanzo,'' alinukuliwa akisema bwana Mende.
M23 wanasema wanataka kuimarisha hali ya maisha ya watu wa mashariki mwa DRC lakini Umoja wa mataifa unasema kuwa wanaungwa mkono na Rwanda, ambayo imekuwa ikijihusisha na nchi hiyo tangu washukiwa wa mauaji ya kimbari ya 1994 kukimbilia nchini humo.

No comments:

Post a Comment