Wednesday, February 27, 2013

Urais 2015: Utafiti wa Synovate wapondwa,wadau wadai una ajenda ya


SHARE THIS STORY
0
Share


BAADHI ya wasomi nchini wameuponda utafiti uliofanywa na Shirika la Synovate huku miongoni mwao wakienda mbali zaidi kwa kusema: “Ulikuwa na ajenda ya siri.”

Utafiti huo pia umepondwa na wanasiasa akiwamo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amesema haziamini tafiti zinazotolewa na Syonovate akidai hazina ukweli wowote.

Licha ya matokeo ya utafiti huo wa Desemba mwaka jana kuonyesha kushuka kwa asilimia 25 kwa umaarufu wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa pamoja na chama chake, lakini unaweka wazi kwamba kiongozi huyu angechaguliwa kuwa Rais kama uchaguzi huo ungefanyika sasa.

Dk Slaa anaongoza kwa asilimia 17, akifuatiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Katika maoni yao, baadhi ya wasomi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini walieleza wasiwasi wao kuhusu usahihi wa matokeo hayo na kuhoji mbinu zilizotumika wakisema inawezekana hazikuwa sahihi.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo ameuponda akisema haukufuata misingi ya sayansi ya siasa.

Dk Makulilo alisema alifanya utafiti kwa kampuni zinazofanya tafiti kama hizo kati ya mwaka 2010 hadi 2011 na kugundua udhaifu mkubwa katika kampuni hizo.

“Kwanza wanakosea, kwa mfano wanaposema kuwa utafiti huu ni mwendelezo wa ule uliofanyika Desemba 5 hadi 18, 2011. Ukichunguza utakuta data hizo hazipo. Zilizopo ni za Mei 2 hadi 19, 2011.”

“Kwa kawaida uelewa wa wananchi wa vijijini ni mdogo ukilinganisha na mijini kwa sababu mijini kuna vyombo vya habari. Kwa mfano, ukiangalia swali la nani anafaa kuwa Rais, mwaka 2011 walisema Dk Wilbrod Slaa alikuwa na asilimia 42, lakini sasa ana asilimia 17.

Vijijini wengi bado wanaikubali CCM kutokana na uelewa mdogo, iweje Dk Slaa ambaye chama chake hakina wafuasi wengi vijijini ashinde?” alihoji.

“Utafiti wa Synovate una dosari kubwa kisayansi, hauonyeshi tarehe wala wapi umefanyika. Waliohojiwa wameonyeshwa umri wao, lakini hawaelezwi maoni yao kulingana na umri, jinsia, wanatoka vijijini na mijini. Nilipofanya utafiti wangu niliwafuata wakakimbia…” alisema Dk Makulilo.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Gaudence Mpangala alisema nyakati za kuelekea Uchaguzi Mkuu, tafiti nyingi hufanyika zikiwa na malengo ya kubeba watu au chama fulani.

Hata hivyo, alisema kilichofanywa na Synovate ni utafiti hivyo kwa kuwa yeye hajafanya utafiti ni vigumu kuupinga moja kwa moja... “Ila kwa mtizamo wa kawaida unatia shaka.”

No comments:

Post a Comment