Saturday, February 23, 2013

Kuziongoza Simba, Yanga yataka moyo


Ili kuwavuta karibu wasomaji, nitahadithia kisa kilichonipata mwaka 1972 nilipokuwa mpangaji katika nyumba namba 7 mtaa wa Mkwaja, Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam.

Nilikuwa na kawaida ya kukaa na mjukuu wetu wa kiume uwani kila siku jioni. Hapo tulipewa chai kwenye vikombe vya plastiki nami kila nilipomaliza chai, nilikirusha kikombe changu juu ya karo lililokuwa jirani. Mjukuu wetu anayeitwa Mwenge, alinitazama kwa makini kila niliporusha kikombe changu kwenye karo.

Kwa silika za kitoto, akadhani ninavyofanya ndivyo itakiwavyo. Siku kadhaa baadaye, alipomaliza chai akarusha kikombe chake karoni! Nilitaka kumkaripia lakini nikasita nilipokumbuka methali isemayo “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Methali hii hutumiwa kuwanasihi wazazi wawalee watoto wao vizuri ndipo wainukie kuwa na tabia nzuri baadaye. Mwenge alizoea kuniona nikirusha kikombe changu baada ya kunywa chai.   

Nachelea kusema mambo yafanywayo na viongozi wa Simba na Yanga, huenda yakavisibu vilabu vingine visivyokuwa na ukomavu. Kama wakongwe (Simba na Yanga) wanafanya hivyo, kwa nini vilabu vilivyoanzishwa baada yao visiige kama alivyoiga mjukuu wetu Mwenge kurushia kikombe kwenye karo?

Toleo la gazeti hili Jumamosi iliyopita nilieleza jinsi kocha wa zamani wa Simba, Milovan Cirkovic alivyorejea nchini kudai fedha zake baada ya mkataba wake kukatishwa kwa njia isiyokuwa ya kiungwana. Siku mbili baadaye, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akamwambia kocha huyo arejee kwao kusubiri fedha atakazotumiwa kupitia akaunti yake ya benki. Milovan anaidai Simba shilingi milioni 50.

Nadhani kwa kutambua ‘ufukara’ (wa kujitakia) wa klabu aliyokuwa akiitumikia (Simba), hakurudi nchini mapema ila alipopata habari kuwa Okwi ameuzwa kwa Waarabu, akaona ndiyo njia pekee ya kulipwa fedha zake. Leo anaambiwa arudi kwao kusubiri fedha zake. Kama hana nauli ya kumrejesha kwao, kulipia chakula na malazi katika hoteli aliyofikia itakuwaje? Bahati nzuri habari za mwishoni mwa wiki zinasema suala lake litafika ukingoni Jumatatu kwa msaada wa Fatma Al Kharous.

Mara nyingi hujiuliza bila kupata majibu sahihi: Huwaje viongozi wa Simba na Yanga kujaribu kuyavuka maji wasiyoweza kuyaogelea? Kwa nini hutaka sifa za kuajiri makocha wa kigeni kwa mishahara mikubwa wasiyoweza kuwapa ilhali hawana vipato zaidi ya viingilio vya mechi? Mbona kuna makocha wazalendo wenye uwezo mzuri wasiokuwa na masharti makubwa kama walivyo makocha wa kigeni?

Yanga ilikuwa ya kwanza kwenda ughaibuni – Uturuki – kwa ziara ya mafunzo ikifuatiwa na Simba iliyokwenda Oman kwa ziara kama hiyo. Ziliporejea nyumbani, magazeti yaliwapamba mno kuwa matunda ya ziara zao yataonekana zitakapoanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Yanga ilipotia timu uwanjani kupambana na Mtibwa ya Turiani inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime, ikaambulia sare ya 1-1 tena ikisawazisha dakika za ‘lala salama!’ Simba nao walibanwa mechi mbili walizocheza dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani na JKT Oljoro ya Arusha kwa sare pia. Mji ukatulia kwani ngebe baina ya pande hizo hazikusikika mitaani!

Jambo la pili ni ushangiliaji wa kishabiki ufanywao na timu za Simba na Yanga wakati mojawapo inapocheza na timu ngeni; na sasa Azam inaathirika kwa ujinga huo. Tuliona jinsi mashabiki wa Yanga walivyojitahidi kuishangilia Al Nasri ya Sudan ingawa mwishowe ilifungwa 3-1 na Azam FC baada ya kuwa mbele kwa bao 1-0 mpaka mwisho wa kipindi cha kwanza. Vilevile tuliona jinsi mashabiki haohao walivyoishangilia Recreativo de Libolo ya Angola na kuishinda Simba 1-0 jijini Dar es Salaam.

Yanga nayo ichezapo na timu ngeni, huwa zamu ya Simba kuwashangilia wageni. Nashindwa kueleza kwa yakini ni kwa nini twapigana vita vya panzi na kuwapa nafasi kunguru kutudonoa watakavyo! Nduguyo anapigwa na mgeni kisha washangilia badala ya kumsikitikia na kumpa msaada? Mbona twajidhalilisha kiasi hiki?

Jambo la tatu ni ahadi zitolewazo na viongozi wa vilabu vya Simba na Yanga ili kuwafurahisha wanachama au wakati wanapoomba kura. Mwishoni mwa mwaka jana, wanachama wa Yanga waliahidiwa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Kaunda mwezi Februari mwaka huu. Wanachama walitakiwa kuchangia kwa hali na mali ili hatua za awali zianze Februari na ujenzi rasmi uanze Juni.

Pamoja na ahadi ile, wanachama hawajajitolea kwa dhati na dalili za ujenzi hazipo! Hata ujenzi wa jengo la ghorofa 10 kwenye makutano ya mitaa ya Mafia na Nyamwezi hauzungumziwi!

Viongozi wa Simba nao waliahidi kujenga ghorofa 12 kando ya jengo lao pale Msimbazi. Mpaka sasa hakuna kinachoendelea, mbali ya mashabiki kujazana pale tangu asubuhi saa 12 wakibishana kwa mambo wasiyoyajua!

Tatizo la wanachama wa Simba na Yanga ni kutozirejelea ahadi wanazoahidiwa na viongozi wao kama zatekelezwa au la; bali muhimu ni ushindi, hasa moja inapoishinda nyingine. Timu inaposhindwa, kizaazaa huanzia uwanjani kama ilivyotokea kwa Ismail Aden Rage kuzomewa na kutukanwa hata akatoka uwanjani kabla ya mechi kumalizika siku Simba ilipofungwa 1-0 na timu ya Angola.

Waingereza husema ‘mpira ni mchezo wa bahati’ na ndivyo ulivyo. Timu yaweza kushindwa nyumbani na mechi ya marudiano ikashinda ugenini. Mwaka 1979 Simba ilifungwa na Mufulira Wanderers ya Zambia mabao 4-0 kwenye uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) jijini Dar es Salaam. Mechi ya marudiano iliyochezwa jijini  Lusaka, Zambia, Simba iliigaragaza Mufulira kwa mabao 5-0, tena mbele ya Rais Kenneth Kaunda!

Timu inaposhindwa, viongozi hutukanwa matusi mazito wakihusishwa wake na wazazi wao! Wendawazimu si kupiga makopo barabarani, kula na kulala jalalani tu. Haya yanayofanywa na Simba/Yanga ‘magoli’ ni wendawazimu tosha! Waungwana hawatukani wala kugombana wanapopatwa na jambo baya.

Katika mashindano kuna kushinda na kushindwa. Ukishindwa, tafuta sababu za kushindwa ili ujirekebishe kwa mashindano yajayo. Kutukana na kufanya fujo hakujengi bali inaonesha tabia za mtu alivyo.

 Aidha ujuha wa kuzishangilia timu ngeni tuuache kwani umetugharimu na unaendelea kutugharimu. Vikombe tunavyogombea na wenzetu wa n-nje tutaishia kuviona kwa macho kama ilivyokuwa Simba iliponyang’anywa tonge mdomoni na Stela ya Abidjan mwaka 1993 jijini Dar es Salaam.

Ilifungwa 2-0 na kukosa kombe mbele ya Rais Ali Hassan Mwinyi huku mashabiki wa Yanga wakishangilia na kuimba “uzalendo umetushinda … uzalendo umetushinda!” Simba ilipata vipigo viwili kwa wakati mmoja. Kwanza kufiwa na mchezaji Hussein Tindwa uwanjani na pili kukosa kombe na kumfanya aliyekuwa mfadhili wake, Azim Dewji, kuporomosha machozi uwanjani.

No comments:

Post a Comment