Friday, May 3, 2013

Madereva wa malori sasa waitishia Serikali



 

Kwa ufupi
Madereva wa malori yanayofanya safari zake ndani na nje ya nchi wametangaza mgomo kwa ajili ya kuishinikiza Serikali kusimamia mikataba ya ajira ambayo mpaka sasa hawajapata.


 Dar es Salaam. Madereva wa malori yanayofanya safari zake ndani na nje ya nchi wametangaza mgomo kwa ajili ya kuishinikiza Serikali kusimamia mikataba ya ajira ambayo mpaka sasa hawajapata.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuunda kamati ya kushughulikia suala hilo ambapo mpaka sasa Serikali na waajiri wao wameshindwa kulitekeleza jambo ambalo limewafanya wawe vibarua wa kudumu.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rocket Matogoro alisema kuwa, mgomo huo utaanza Mei 10 mwaka huu ambapo madereva hao hawataendesha magari hayo mpaka suala hilo litakapotekelezwa. “Madereva wa malori tumeandaa mgomo ili kuishinikiza Serikali kusimamia mikataba yetu ya ajira ambayo mpaka sasa imekuwa hewa, jambo ambalo linatufanya waajiri watudharau,”alisema Matogoro.
Alisema kutokana na hali hiyo madereva hao siku hiyo hawataondoa magari katika maegesho mpaka suala hilo litakapomalizwa. Mbali na hilo,madereva hao wameitaka Serikali kujenga maegesho ya magari katika vituo ambavyo vimepangwa ili kuondoa usumbufu unaojitokeza sasa.

No comments:

Post a Comment