Wednesday, April 10, 2013

Miili ya polisi waliouawa Nigeria yapatikana



 
Eneo la Niger Delta

Maafisa wa usalama nchini Nigeria wamepata miili 11 ya wanajeshi 12 waliouawa katika eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Niger Delta siku ya Ijumaa.
Polisi wanasema kuwa baadhi ya miili hiyo ilikuwa imekatwakatwa na kuchomwa kiasi cha kutotambulika.
Wiki jana kundi moja la wapiganaji, lilisema kuwa litaanza mashambulizi mapya baada ya kiongozi wake Henry Okah, kufungwa jela kwa kufanya shambulizi la bomu mwaka 2010.
Eneo hilo lenye utajiri wa mafuta, ni muhimu sana kwa uchumi wa Nigeria.
Hata hivyo, watu wengi ni maskini na hivyo huchukizwa na serikali pamoja na makampuni ya mafuta kwa kutowafaidisha na rasilimali hiyo.
Mwishoni mwa wiki, kundi la wapiganaji wa MEND, walisema kuwa walivamia mashua iliyokuwa imewabeba polisi katika jimbo la Bayelsa na kuwaua polisi.
Msemaji wa polisi, Alex Akhigbe alisema kuwa miili 11 zilipatikana wakati polisi mmoja hajulikani aliko.
Miili hiyo ilisafirishwa kwa boti hadi katika eneo la Yenagoa ambao ni mji mkuu wa jimbo hilo kuchukuliwa na familia zao.
Aidha mwishoni mwa wiki polisi walikana kuwa mauaji hayo yanaweza kuhusishwa na kufungwa kwa Henry Okah.
Badala yake walisema kuwa yalihusu mgogoro wa malipo ya mishahara ya wapiganji hao waliokuwa wanalipwa baada ya kukomesha harakati zao za mapigano dhidi ya serikali.
Mashua za polisi waliokuwa wanamsindikiza mwenzao kwa mazishi, zilikumbwa na hitilafu na hivyo kulengwa na wapiganaji hao kwa mashambulizi.
Kundi la Mend lilikuwa linafanya vurugu kutaka kupewa sehemu ya rasilimali za mafuta Kusini mwa Nigeria lakini likasitisha harakati zao mwaka 2009, wakati waliposalimisha silaha na kusamehewa.

No comments:

Post a Comment