Thursday, March 7, 2013

Tume ya uchaguzi Kenya kushtakiwa



 
Tume ya uchaguzi ingali inatangaza matokeo ya urais leo bunge moja baada ya nyingine

Muungano wa CORD wake Raila Odinga unapanga kwenda mahakamani kutaka mahakama kusitisha shughuli ya kuhesabu kura za urais inayoendelea katika ukumbi wa Bomas.
Chama hicho kinasema kuwa matokeo ya mgombea wao yanahujumiwa katika ukumbi huo wakidai wizi wa kura.
Madai haya waliyatoa hapo jana ingawa mkuu wa tume ya uchaguzi aliyakanusha vikali na kusema hakuna mahala popote ambapo wameshuhudia matokeo kuhujumiwa.
Chama hicho pia kilidai kuwa baadhi ya matokeo yalikuwa juu ikilinganishwa na idfadi ya wapiga kura.
Na kwa hilo, mkuu wa tume ya uchaguzi Isaack Hassan pia alikanusha vikali akisema hawajapata matokeo kama hayo.
Tume hiyo imesisitiza kuwa shughuli ya kuyahakiki matokeo infanywa mbele ya maajenti wa vyama vyote.
Wakati huohuo tume hiyo imekiri kuwa kulikuwa na tatizo la mtambo wake wa kupeperusha matangazo ikisema kuwa ilikuwa inaongeza mara nane kura zilizoharibika.
Washika dau wengi walieleza wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya kura zilizoonekana kuharibika kwani zilikuwa kura zaidi ya laki tatu. Lakini kufikia sasa zimepungua na kufika themanini.
Mkuu wa tume hiyo, Issack Hassan alisema kuwa komputa ilikuwa inaongeza idadi ya kura zilizoharibika kwa mara nane.
Shughuli ya kukusanya matokeo ilianza upya kwa mikono kufuatia matatizo haya lakini Uhuru Kenyatta angali anaongoza dhidi ya Raila Odinga.
"kulikuwa na makosa kwa namna ambavyo programu ya komputa ilikuwa imeundwa, '' alisema Hassan.
''Kwa kura zote zilizoharibika kwa kila mgombea zilikuwa zinaongezeka mara nane ,'' aliongeza kusema mwenyekiti wa tume ya uchaguzi.

No comments:

Post a Comment