
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
Aidha, CCM kimemtupia lawana Maalim Seif kwamba anafanya vitendo vya kuhatarisha amani visiwani humo.
Akihutubia mamia ya wanachama na mashabiki wa CCM waliohudhuria
mkutano wa hadhara uliofanyika Jumba la Vigae huko Jang’ombe mjini hapa
jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alidai kuwa
Maalim Seif ameanza kufanya vikao vya siri vinavyotishia kuvuruga amani
na umoja wa kitaifa visiwani humo.
Vuai ambaye ni kati ya wajumbe walioshiriki katika mchakato wa
mazunguzmzo yalioleta upatanishi na kufikia mwafaka wa kisiasa Zanzibar,
alisema kama angejua mapema dhamira ya Maalim Seif katika mazungumzo ya
kundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, angekuwa radhi kujitoa katika
mazungumzo ya kufikia mwafaka.
Alisema kwamba hivi karibuni Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa
CUF, aliitisha kikao maalum cha vijana wa chama chake na kusema kuwa
ikiwa chama chake kitawaamrisha vijana kufanya vurugu, nchi
haitatawalika na ikibidi jahazi litote na kujaa maji.
“Msingi wa mazungumzo yetu katika awamu zote za kusaka maridhiano
ya kisiasa yalihimiza kujengeka kwa amani, utulivu kuimarisha misingi ya
umoja wa kitaifa,” alisema.
Vuai aliiita kauli hiyo ni ya kichochezi na kwamba haikubaliki
mbele ya jamii hivyo aliwatolea wito viongozi wa kisiasa na kiserikali
kuchunga ndimi zao ili kuyaenzi mazingira yaliyoleta amani, umoja na
utulivu uliopo visiwani hapa.
“Kama anahitaji jahazi litote tugawane mbao ni heri akachukua
mapema ubao wake na kuelekea Mtwambwe (Pemba), lakini hatuko tayari
kuona amani ya Zanzibar ikichezewa na kupotezwa kwa maslahi binafsi,”
alisema Vuai.
Vuai aliendelea kudai kuwa miongoni mwa mambo waliokubaliana katika
mchakato wa mazungumzo ya kusaka mwafaka ni kuwaasa wanasiasa wasitoe
kauli na matamshi makali yanayoweza kuibua mpasuko wa kisiasa.
Alisema kwa muda wa mwaka mmoja CCM kimekuwa hakifanyi mikutano ya
hadhara kwa kuheshimu makubaliano hayo, lakini cha ajabu viongozi wa CUF
wamekuwa wakiendesha mikutano yenye lengo la kuirudisha nyuma Zanzibar.
Akizungumzia madai ya kuwepo kwa utata katika Muungano, Vuai
alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni halali na kuwataka
wanasiasa wanaopotosha jambo hilo kukaa na kutafakari kwa kina faida
zitokanazo na kuwapo kwake na athari ikiwa Muungano huo utavunjika.
“Ikiwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utavunjika, nafikiri
huenda hata utulivu na maelewano kati ya Unguja na Pemba nayo yanaweza
kutetereka, wanaopigia debe na kulishabikia jambo hilo litokee
wanahitaji kupima pepo za nyakati na ikibidi waepukwe badala ya
kuwashabikia,” alisema Vuai.
Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Idara ya
Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu, alisema sera ya CCM
katika Muungano ni kuendelea na mfumo wa serikali mbili na kwamba hakuna
mpango wa kuwa na serikali ya mkataba au kuvunja Muungano uliopo.
NIPASHE ilimtafuta Maalim Seif jana ili kujibu madai hayo, lakini mara zote alizopigiwa simu yake iliita bila kupokelewa.
Katibu wake, Issa alipoulizwa na NIPASHE jana alisema hawezi kujibu
lolote kwa kuwa madai hayo yalitolewa katika jukwaa la siasa na yeye ni
msaidizi wa Maalim Seif upande wa serikali.
Hivyo akashauri aulizwe Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Salim Bimani.
No comments:
Post a Comment